Mfumo
wa mmeng’enyo wa chakula katika mwili unaohusika na umeng’enyaji wa
chakula mpaka kuwa katika hali inayoweza kusharabiwa na mwili ili
kuuwezesha kufanya kazi mbalimbali.
Sehemu
kuu zinazohusika katika umeng’enyaji huo ni kinywa, umio/esofagasi
(ujia wa msuli wenye urefu wa sentimeta 23 ambao huunganisha koromeo na
tumbo), mfuko wa tumbo, ini, mfuko wa nyongo, duodenamu (sehemu ya
mwanzo ya utumbo mdogo inayoanzia katika pilorasi ya tumbo).
Nyingine
ni iliamu (utumbo mdogo kati ya jejunamu na sikamu), kongosho, utumbo
mpana na rektamu (sehemu ya mwishoni ya utumbo mkubwa yenye urefu wa
sentimeta 13, rektamu huanzia mwishoni mwa koloni ya sigmoidi na kuishia
mwanzoni mwa unyeo).
Mfumo
wa mmeng’enyo wa chakula hasa kuta za umio, tumbo na utumbo mwembamba
hupata mmomonyoko ambao husababishwa na asidi inayotumika kumeng’enya
chakula inaposhambulia kuta hizo. Kitaalamu hali hii hutambulika kama
‘Peptic Ulcers’.
Vidonda
vya mfumo wa umeng’anyaji chakula vikiwa kwenye tumbo tunaita vidonda
vya tumbo ‘Gastric Ulcer’, vikiwa katika duodenamu tunaita ‘Duodenal
Ulcer’ na vikiwa katika esofagasi tunaita ‘Esophageal Ulcer’
Nini husababisha vidonda vya tumbo?
Kisababishi
kikuu ni bakteria aina ya helicobacter pylori ni kupitia vyakula na
maji. Pia, hupatikana kwenye mate ya binadamu hivyo inaweza kusambazwa
mdomo kwa mdomo kama wapenzi wanaonyonyana ndimi.
Bakteria hao huishi kwenye kuta za utumbo na hutengeneza vimeng’enya viitwayo urease inayopunguza athari za asidi kwenye utumbo.
Utumbo hutaka kufidia kiasi cha asidi kinachopotea kwa kutengeneza zaidi na husababisha kukwangua kuta za utumbo.
Sababu
nyingine ni chembe za urithi genetics. Idadi kubwa ya watu wenye
vidonda vya tumbo wana ndugu wa karibu na wenye vidonda pia. Hii
huwafanya wataalamu kufikiria kuwa chembe za urithi zinahusika pia.
Uvutaji
sigara na tumbaku. Wavutaji wa sigara wako katika hatari ya kupata
vidonda vya tumbo ikilinganishwa na wasiovuta. Matumizi ya pombe/vilevi.
Walevi wako katika hatari zaidi ya kupata vidonda vya tumbo
ikilinganishwa na wasiotumia vileo.
Msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo hausababishi vidonda moja kwa moja ila hufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa wagonjwa.
Dalili za vidonda
Ieleweke
ni mara chache mtu kuugua vidonda vya tumbo na kutoonyesha dalili.
Zifuatazo ni dalili zinazotokea kwa wagojwa wengi; maumivu ya tumbo na
huwa makali zaidi pale asidi inapopita juu ya vidonda. Maumivu yanaweza
kuanzia kwenye kitovu na kupanda juu hadi katikati ya kifua. Maumivu
yanaweza kuongezeka unapokuwa njaa. Pia, yanaweza kuwa makali wakati wa
usiku yanayoweza kupunguzwa kwa kula chakula kidogo.
Dalili
nyingine ni kushindwa kumeza vizuri chakula au kukwama kama kinataka
kurudi mdomoni, kujisikia vibaya baada ya kula, kupungua uzito, kukosa
hamu ya kula.
Dalili hatari ni pamoja na kutapika damu, kupata choo kikubwa cheusi au chenye damu nzito na kupata kichefuchefu na kutapika.
Jinsi ya kugundua vidonda vya tumbo
Maelezo ya mgonjwa kuhusu dalili humsaidia daktari kuhisi kinachomsumbua mgonjwa kuwa ni vidonda vya tumbo.
Ili
kuthibitisha vidonda vipimo vifuatavyo hufanyika. Kupima damu kuangalia
bakteria aina ya h.pylori na kama mgonjwa amekuwa akitumia antibayotiki
au dawa za vidonda Proton Pump Inhibitors ‘PPIs’ mfano Omeprazole.
Vipimo vyake vya damu vitaonyesha majibu hasi.
Kupima
pumzi. Mgonjwa hupewa anywe maji yenye atomi za kaboni zinazoweza
kuvunjika, hii hufanya bakteria H.pylori kuvunjika na baada ya saa moja
mgonjwa hutoa pumzi kwenye chombo kilichofunikwa. Ikiwa mgonjwa
ameambukizwa sampuli ya pumzi itaonyesha vipande vya kaboni kwenye
kabonidioksaidi.
Kupima
antijeni kwenye kinyesi. Kipimo hiki huangalia kama kuna bakteria
h.pylori kwenye kinyesi. Vilevile kipimo hiki hutumika kuangalia ufanisi
wa matibabu yaliyotolewa dhidi ya bakteria.
Kufanya
x-ray ya sehemu ya juu ya tumbo ‘upper gastrointestinal x-ray’. Picha
huonyesha ‘esophagus’, mfuko wa tumbo ‘stomach’ na dudenum. Mgonjwa
humeza maji yenye ‘Barium’ ambayo hufanya vidonda kuonekana kirahisi
kwenye x-ray.
Matibabu
Kama vidonda vitakuwa vimesababishwa na bakteria h.pylori dawa za kuua na kuondoa bakteria hutumiwa.
Kama
vidonda vya tumbo vitakuwa vimesababishwa na ‘NSAIDs’ na hana
maambukizi ya bakteria h.pylori atapaswa kutumia dawa Proton Pump
Inhibitors ‘PPIs’ mfano Omeprazole, Esomeprazole & Lansoprazole.
Proton
Pump Inhibitors ‘PPIs’ hufanya kazi kwa kuvunja/kuzuia kazi ya protini
ziitwazo ‘Proton Pump’ ambazo huhusika katika utengenezaji wa asidi
tumboni.
Matumizi ya NSAIDs kwa ajili ya kuondoa homa na maumivu yatarithiwa na dawa kama Paracetamol.
Vilevile dawa aina ya H2-Receptor Antagonists mfano Cimetidine, hutumika kama mbadala kama dawa aina ya ‘PPIs’ hazitokuwepo.
H2-Receptor
Antagonists hufanya kazi ya kuzuiia utendaji wa protini iitwayo
‘Histamine’ ambayo inahusika na kuchochea utengenezaji wa asidi tumboni.
Matibabu
yaliyozungumziwa hapo juu yanaweza kuchukua muda kabla ya kuanza
kufanya kazi, hivyo daktari anaweza kuongeza matibabu mengine kama
vizuia asidi ‘Antiacids’ & ‘Alginates’ kwa ajili ya nafuu ya haraka.
Namna ya kuishi na vidonda vya tumbo
Mambo
yafuatayo yatakusaidia kuishi vizuri ukiwa na vidonda vya tumbo;kuacha
kutumia kahawa na chai, kwani vitu hivi huongeza kiwango cha asidi
kinachotengenezwa na tumbo lako. Unaweza kutumia chai ya mitishamba kama
mbadala.
Kunywa maziwa na vitu vitokanavyo na maziwa kama maziwa mgando na jibini.
Maziwa
hufikiriwa kufunika utumbo na kupunguza athari za asidi ya tumboni.
Jitahidi kupunguza uzito hasa ikiwa uzito umezidi na hauendani na kimo
chako.
Kula angalau kidogo mara kwa mara. Hii itasaidia kupunguza athari za asidi inayotengenezwa na tumbo.
Acha
au kunywa vileo siku maalumu tu kwa maana unywaji wa pombe mara kwa
mara hutonesha kwenye vidonda vya tumbo vinavyotaka kupona.
Epuka matumizi ya viungo vya vyakula kwa maana hufanya hali kuwa mbaya zaidi.
Acha
kuvuta sigara, tumbaku, na bangi. Uvutaji wa sigara utakuweka kwenye
hatari zaidi ya kuanza vidonda vipya na kuzuia vidonda vingine visipone.